UKABILA NI NINI?

UKABILA NI NINI?
Viongozi wa nchi ya Kenya ni viumbe wa ajabu sana. Mwanzo mghala muue na haki umpe, Vigogo hawa wamebarikiwa kwa kipawa kimoja; ushawishi wa maneno. Iwapo baadhi yao wangekuwa wahubiri wa injili basi ni wachache sana wangeukosa ufalme wa binguni.

Tangu zama za mwenda zake Adolf Hiltler , Yule kiongozi mkatili wa Ujerumani, ulimwengu haujashuhudia kiongozi aliyeweza kuyatawala mawazo ya wananchi wenzake kwa kiasi alichofikia huyu baradhuli wa chama cha Nazi. Ila watawala wa siasa za Kenya wanampa Hitler changamoto kubwa. Viongozi wa Kenya wanatishia kuivunja rekodi ya Hitler kwa utumizi wa porojo na chuki kama chombo cha kujinyakulia na kusalia kwenye mamlaka.

Waheshimiwa nchini Kenya wamebarikiwa kwa ufasaha wa maneno, vichekesho na matusi ila upungufu nao upo. Upungufu wenyewe hudhihirika wakati wanapohitajika kuambatanisha maneno na vitendo. Ni nadra sana kwa viongozi wa Kenya ‘kusema na kutenda’ jinsi wanavyojidai kwenye majukwaa ya siasa.

Ukilitazama swala la ukabila kwa umakini, kila mwanasiasa wa Kenya atahubiri umoja wa kitaifa (Ijapokuwa Ababu Namwamba anayehubiri umoja wa wazungumza kiluhya). Lakini heri anayehubiri na kunywa mvinyo kuliko anayehubiri sharubati na kunywa mvinyo.

Fauka ya wanayoyasema, akina Uhuru, Ruto , Kalonzo na Raila wamepata umaarufu wa kisiasa kupitia njia mbovu na potovu ya ukabila. Musalia wa Mudavadi naye anazidi kujongeajongea kwenye hili jukwaa la chuki na migawanyiko ya kikabila. Wote hawa wanajidai eti wao ni viongozi wa kitaifa lakini hakuna hata mmoja wao anayeweza kusema alivyosema mheshimika hayati Julius Nyerere kuwa ‘ukabila ni upumbafu.’ Wakisadifu kuyasema hayo, pindi tu wakimaliza usemi, vitendo vyao vya mapendeleo na ubaguzi wa kikabila vitawahukumu. Hatuna budi kuwaheshimu wahenga waliosema kuwa ada ya mja hunena, muungwana ni kitendo.

Hivi basi, ukabila ni nini?

Ukabila ni hali ya kimawazo inayomwongoza mja kuamini kuwa kabila lake ni la kipekee. Hali hii bila shaka humfanya mtu kuwa na kiburi . Akishakijaza kichwa chake kasumba hii, basi mapenzi yake kwa kabila lake hugeuka na kuwa chuki kwa yeyote asiyekuwa na ‘bahati’ ya kuzaliwa kwenye kabila hilo teule. Mwishowe huyu kiumbe atajenga imani kuwa kiongozi wa kabila lake asipotawala, wale ‘wadhaifu’ wa makabila mengine wataiharibu nchi. Huu ni upumbafu wa kiasi kikubwa sana.

Siamini kuwa ukabila unaletwa na maarifa ya mwanasiasa pekee. Ukabila ni hisia tunayozaliwa nayo. Mwanasiasa kwa ajili ya ‘uerevu’ wake hutafuta mafuta ya petroli akayanyunyiza kwenye makavu ya ukabila na kuwasha kiberiti. Hapo ndipo moto wa chuki huwaka, naye mwanasiasa husalia akijigamba kuwa yeye ni fahali. Kwa sababu ukabila ni ushenzi wa asilia, hata masomo hushindwa kuliondoa doa hilo. Hivyo basi haishangazi tena kuwaona vijana wachanga kwenye vyuo vikuu wakitapatapa kwenye huu uchafu wa kikabila na kugaragara kama nguruwe walio punguani. Wao hunena bila aibu kwenye mitandao kuwa kiongozi wa kabila lake eti ndiye anastahili kutawala Kenya. Maoni yangu ni kuwa huu ni ushenzi mtupu.

Siasa za Kenya hazina kikomo. Kila wakati tunayaweka masaa mengi sana kwenye malumbano ya kisiasa. Tayari, hawa vigogo wameanza kupimana nguvu wakilenga kujiongezea umaarafu kabla ya uchaguzi wa 2017. Tangu serikali ya Rais Daniel Toroitich Arap Moi ilipolegeza sheria na kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, ukabila umeimarika.Sikumpenda sana rais Moi lakini namheshimu kwa hekima yake alipobashiri kuwa mfumo wa vyama vingi ungeleta migawanyiko ya kikabila. Hilo limefanyika. Ambalo halijafanyika ni hali ya kila mkenya kuukumbatia ukabila. Mimi ninahesabika kati ya hawa wananchi wanaosherehekea utaifa. Hili nalo lahitaji nguvu nyingi mithili mwogeleaji anayeogelea kwa kupingana na mkondo wa maji ya mto kama vile Nzoia au Tana. Asipoupiga moyo konde atabadislisha mwelekeo alivyofanya mheshimika Koigi wa Wamwere. Furaha yangu ni kwamba kunao wakenya wengi wanaoendeleza uasi dhidi ya ukabila.

Kunao wazaliwa wa Kenya ya kati wanaosema kuwa sio lazima mkikuyu atawale Kenya. Sio lazima mkamba atawale. Sio lazima mjaluo aingie ikulu. Sio lazima ikuwe eti ni Kalenjin au maasai au mluhya au mkisii. Sio lazima awe islamu au mkristo. Sio lazima awe mzaliwa wa pwani au mfugaji wa kuhama kutoka eneo la Turkana. Si lazima. Inawezekana pia iwe mkuria au mteso au jamaa kutoka bara hindi au hata Yule ambaye wazazi wake walikimbilia Kenya kutoka South Sudan naye akawa mwananchi wa Kenya kwa haki ya kuzaliwa. Inawezekana iwe muhindi ambaye wazazi wake waliingia Kenya kama wajenzi wa reli zaidi ya miaka mia moja iliopita achaguliwe kama rais wa Kenya. Kunao wakenya wanaosema kwa vinywa na mioyo yao kuwa haijalishi ni kabila gani, mkenya ni mkenya na wakenya wote ni sawa. Ukifikia pale umejikomboa.

Ukombozi wa kwanza, tuliwafukuza walowezi kutoka uropa tukajivunia kuwa waafrika huru. Ukombozi wa pili, tuliamua kujitawala kwa njia ya vyama vingi vya kisiasa. Tukasherehekea demokrasia. Ukombozi wa tatu utapatikana pale ambapo wakenya watashinda vita dhidi ya ukabila na kuwachagua viongozi kwa vigezo vipya. Hapo ndipo taifa la Kenya litastawi kwa kiasi cha kila mwananchi kufurahia matunda ya kazi yake. Hapo ndipo mzaliwa wa kibera, Mathare, Kangemi na Mukuru atashawishika kufanya bidii ya kujiondoa kwenye umaskini kwani atafahamu kuwa fanaka haiji tu kwa bahati na sibu ya sportpesa. Tutajua kuwa ukombozi wa tatu umefika wakati ambapo, itakuwa nadra sana kukutana na mtu maskini. Wakati ambapo makao yanayoitwa ‘vitongoji duni’ hayatakuwepo tena na magereza kukosa wafungwa kwani uhalifu utakuwa umedidimia. Hayo yote ni ya baadaye lakini mwanzo ni kupambana na ukabila kwa udi na ambari.

Kuzama kwa ukabila ndiko kuzaliwa kwa UKOMBOZI WA TATU

Advertisements